KUNDI zima la muziki wa bongo fleva TMK Wanaume Family lenye
maskani yakeTemeke jijini Dar es Salaam, litasindikiza utambulisho wa
msanii chipukizi wa muziki huo Aslahi Isihaka ‘Dogo Aslay’
litakalofanyika Juni 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma na
baadaye Ukumbi wa Royal Village mjini humo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam jana
mratibu wa onesho hilo Jackline Masano wa Kampuni ya Ruhazi Promotion ya
jijini Dar es Salaam, alisema kuwa TMK Family wamepatia kutoa burudani
ya uhakika katika onesho hilo.
Alisema TMK Family wataungana na wasanii kutoka kituo cha Mkubwa na
Wanawe cha Temeke Sandali jijini katika kumsindikiza msanii huyo aliye
gumzo hivi sasa kutokana na wimbo wake ‘Naenda Kusema’.
“Tunawaomba mashabiki na wapenzi wa muziki huo mjini Dodoma na
maeneo jirani kwamba kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Jamhuri
kuanzia saa 6:00 mchana mpaka saa 12:00 jioni, na kisha kwenye Ukumbi wa
Royal Village kuanzia 2:00 usiku hadi saa 6:30 ,” alisema Jackline.
Jackline aliongeza kuwa pamoja na onesho hilo kupambwa na wasanii
wengi lakini kiingilio kitakuwa shilingi 5,000 tu kwa wakubwa na
shilingi 1,000 kwa watoto ili kuwawezesha wapenzi wengi zaidi kukimudu
ambapo watapata burudani ya uhakika.
Aidha, Jaqueline aliongeza kuwa kampuni yao inaendelea na mazungumzo
na wasanii wengine ili kuweza kusindikiza maonesho hayo yote na pindi
mazungumzo yatakapokamilika watawaweka hadharani.
No comments:
Post a Comment