Friday, May 18, 2012

BURIANI PATRICK MUTESA MAFISANGO




Gari alilokuwa akiendesha marehemu Patrick Mafisango. picha baada ya ajari



  MWILI wa kiungo mahiri wa SImba SC, Patrick Mutesa Mafisango (32), sasa utaagwa kwenye Uwanja wa TCC, Chang'ombe, Dar es Salaam, kuanzia saa 3:00 asubuhi badala Leaders Club, Kinondoni, kama ilivyotangazwa awali.

Mafisango amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika eneo la Keko jirani na Chuo cha VETA jijini Dar es Salaam.
Mafisango alikufa kutokana na ajali iliyotokea wakati gari alilokuwa akiendesha lilipogonga mti ulio pembezoni mwa barabara ya Chang’ombe majira ya saa kumi kasorobo alfajiri. Marehemu alifariki papo hapo.
Kwenye gari aliyokuwamo Mafisango, kulikuwapo na abiria wengine wanne lakini ni Mafisango pekee ndiye aliyefariki dunia.
Mwili wa Marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tayari kwa kusafirishwa kwenda kwao Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako atazikwa.
Ingawa alikuwa na uraia wa Rwanda na akiichezea timu ya taifa ya nchi hiyo (Amavubi), Mafisango alikuwa ni mzaliwa na raia wa DRC na uamuzi wa kuzikiwa huko ni wa familia yake.
Msiba wa Mafisango uko katika eneo la Keko Toroli jirani na kituo cha Chang’ombe Maduka Mawili (Njia Panda Sigara).
Mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa leo Ijumaa saa nne asubuhi katika uwanja wa TCC, Chang'ombe  jijini Dar es Salaam kabla ya mwili wake kusafirishwa kwenda Kinshasa majira ya saa kumi jioni.

Mafisango alizaliwa Machi 30, 1980 huko Kinshasa Zaire wakati huo na ameacha mke na mtoto mmoja wa kiume, Chris Paul, mwenye umri wa miaka mitano.
Mafisango ameichezea Simba kwa msimu mmoja tu akitokea Azam ya Dar es Salaam lakini kabla ya hapo alichezea pia TP Mazembe ya DRC, APR ya Rwanda na pia aliwahi kuwa nahodha wa Amavubi kwa takribani miaka mitano.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, Makamu wake, Geofrey Nyange Kaburu na wajumbe wa kamati ya watendaji wameeleza kusikitishwa kwao na msiba huu mkubwa kwa klabu na wamewataka wana Simba wote kuwa watulivu na kumwombea marehemu.

 Mungu amlaze mahali pema peponi.





1 comment:

  1. RIP Patrick.

    Simba has lost a true player for real...

    ReplyDelete