MICHUANO ya mchezo wa pool vyuo vikuu kitaifa yamemalizika mjini
hapa kwenye ukumbi wa Welfare huku Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine
kikiibuka kidedea.
Mashindano hayo yaliyoanza Mei 26 hadi Mei 27 yalishirikisha timu
kutoka vyuo vya Mtakatifu Augustino cha Mwanza, Mtakatifu John Dodoma,
TIA kutoka Mbeya, Mzumbe Morogoro, IFM Dar es Salaam, MUCOBS Kilimanjaro
na AIA cha jijini Arusha huku wenyeji wao wakiwa Chuo Kikuu cha Ruaha,
(RUCO), cha mjini hapa.
Mabingwa hao, Mtakatifu Augustine, walifuatiwa na IFM, RUCO na UDOM.
Kwa ushindi huo, Chuo cha Mtakatifu Augustine kilijitwalia kitita cha
sh 2,500,000 pamoja na kombe, mshindi wa pili IMF alizawadiwa sh
1,500,000, mshindi watatu RUCO sh 1,300,000 wakati washindi wa nne UDOM
ilijipoza na sh 1,000,000.
Pia zilitolewa zawadi za mshindi mmoja ambako kwa wanaume.
Pia kulikuwa na zawadi kwa washindi mmoja mmoja, ambapo kwa upande wa
wanaume zilikwenda UDOM sh 300,000, MUCOBS sh 200,000, RUCO sh 150,000
na IFM sh 100,000.
Kwa upande wa wanawake zilikwenda IFM sh 200,000 UDOM sh 150,000, MUCOBS sh 100,000 na AIA sh 50,000.
Timu nne za mwisho, TIA Mbeya, Mzumbe Morogoro, MUCOBS na AIA zijipatia kifuta jasho cha sh 500,000 kila timu.
Akitoa zawadi hizo, Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi,
aliipongeza Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kwa mchango wao mkubwa katika
kuinua vipaji vya vijana katika michezo mbalimbali, huku akiwaasa wadau
wa michezo kuwa ni vema wakaingia katika michezo yote na sio kufikiria
soka tu, kwani itawapa nafasi ya wananchi kuchagua mchezo wanaoupenda.
Pia aliwaasa wapenzi wa mchezo huo na mingine yote, kutocheza wakati
wa kazi kwani hata pool umekuwa ukionekana wa kihuni kutokana na watu
wengi kucheza wakati wa kazi na kuzorotesha maendeleo ya taifa.
“Pool table awali kwa mtazamo ulikuwa unaonekana kuwa mchezo wa
kihuni, lakini si sahihi. Kwa ufuatiliaji na maelezo ya wahusika ni
mchezo wa pili kwa kupendwa kutoka mchezo wa mpira wa miguu kwa sasa.
Mimi nimependezwa sana na huu mpira uliochezwa kwa kushirikisha vyuo,
kwani vijana wameweza kukutana pamoja na kuzungumza mambo yanayowahusu,”
alisema Mwamwindi.
Michuano hiyo ilidhaminiwa na TBL kupitia bia yake ya Safari Lager.
CHANZO CHA HABARI: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment