TIMU za soka Tanzania ‘Kilimanjaro Stars’ na Malawi ‘The Flames’
 jana zimeshindwa kutambiana baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana
 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa
 jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ulikuwa ni mahususi kwa timu hizo kujinoa kwa ajili ya 
mechi zake za mchujo wa kuwania kucheza Kombe la Dunia Juni 2, ambapo 
Stars itakuwa Ivory Coast, huku Malawi  itakwaana na Kenya ambapo zote 
zitacheza ugenini.
Katika mchezo wa jana timu timu hizo zilionekana kusomana zaidi ambapo
 wachezaji wake walijaribu kufanya mashambulizi ya hapa na pale lakini 
hayakuleta matunda yoyote.
Dakika ya 33 Joseph Kamwendo wa Malawi alikosa bao la wazi baada ya shuti lake kugonga mwamba.
Dakika ya 40 Kazimoto naye alishindwa kutikisa nyavu za Malawi baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa,  Simplex Nthala.
Mwamuzi wa kimataifa, Oden Mbaga, alimlima kadi ya njano Kamwendo katika dakika ya 43 baada ya  kumchezea vibaya Kazimoto.
Malawi ilionekana kuishambulia zaidi Stars lakini jitihada za Kipa 
Juma Kaseja ziliwezesha kuzuia nyavu zake kutikiswa. Hivyo kipindi cha 
kwanza kumalizika kwa sare 0-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikionekana kuwa na 
uchu wa kupata bao ambapo katika harakati hizo mshambuliaji wa Stars 
Mbwana Samatta alikosa bao la wazi katika dakika ya 58 baada ya shuti 
lake kutoka nje.
Mbaga alimzawadia kadi ya njano nyota wa The Flames, James Sangala, baada ya kumchezea vibaya Samatta.
Katika mchezo huo Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya bia Tanzania 
(TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro ilimtoa Wazir Salum na kumuingiza 
Amir Maftah, huku The Flames ikiwatoa Dave Banda, Zicco Mkanda, Russell 
Mwafulirwa na kuwaingiza Jimmy Zakazaka, Amadu Ally na Ndaziona 
Chatsalira.
Katika mchezo ambao hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu iliyoweza 
kuliona lango la mwenzake, Kili Satrs inayonolewa na Mdenish Kim 
Poulsen,  ambaye jana ilikuwa ni kibarua chake cha kwanza tangu arithi 
mikoba ya Mdenish mwenzake, Jan Poulsen, ilionekana na mabadiliko 
makubwa na hasa wachezaji wake kuonekana wamepikwa vema.
Hata hivyo chipukizi waliomo katika kikosi cha Stars kama Frank Domayo
 walionekana kutozoea mikiki, huku safu ya kiungo ikionekana 
kutowasiliana vema na washambuliaji, wakati nafasi ya ulinzi nayo kidogo
 ilionekana kuzubaa.
Stars: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Wazir Salum/Amir Maftah, Aggrey 
Morris, Kelvin Yondan, Shaban Nditi, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana 
Samatta, Haruna Moshi ‘Boban’ na Mwinyi Kazimoto.
Malawi: Simplex Nthala, Limbikani Mzava, Moses Mvula, Foster Namwela, 
James Sangala, Joseph Kamwendo, Frank Banda, Dave Banda/Jimmy Zakazaka, 
Zicco Mkanda/Amadu Ally, Robin Ngalande na Russell Mwafulirwa/ Ndaziona 
Chatsalira.
No comments:
Post a Comment