Monday, June 11, 2012

Wasanii watakiwa kuiga kutoka Ghana

WASANII wa muziki nchini, wametakiwa kuiga mipangilio ya maendeleo kutoka nchini Ghana, ili kufikia mafanikio na kuachana na vilio vya kuibiwa kazi zao kila siku.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mkurugenzi Msaidizi wa Rulu Arts Promotions, Angelu Luhala, alisema Ghana wamejipanga vilivyo kudhibiti wizi wa kazi za wanamuziki na kwa asilimia kubwa wamefanikiwa.

Luhala alikuwa nchini Ghana kwa mwaliko wa Kampuni ya Best AC ambayo inashirikiana na Rulu Arts, ambako pamoja na mambo mengine, alijionea mifumo makini ya kudhibiti wizi wa kazi za wanamuziki.
Alisema Ghana wamefanikiwa kimuziki kwa sababu wanamuziki wake wana umoja wa kweli, na serikali inawapa sapoti kubwa.

Aidha, Luhala alisema Serikali ya Ghana imekuwa ikitenga Euro milioni 2 kila mwaka kwa ajili ya utafiti katika sekta ya muziki kama moja ya maeneo yanayoweza kutoa ajira kwa vijana na jamii kwa ujumla.

Luhala alisema serikali ya Ghana imeunda vyama vinne ambavyo vinasaidia wanamuziki ambavyo ni pamoja na GAPI kinachohusika na uzalishaji, usimamizi na usambazaji wa kazi za wanamuziki na GAMRO inayohusika na ukusanyaji wa mirabaha katika kumbi za muziki, vituo vya redio, magari na maonesho ya majukwaani.

Chama kingine ni MUSIGA ambacho wanamuziki wanafanikiwa kupitia sheria namba 690 ya mwaka 2005 inayounda ofisi ya hakimiliki na utawala wa hakimiliki na timu ya kudhibiti kazi za wanamuziki wakiwemo wanasheria, polisi, wapelelezi na wanamuziki.
Na  na Khadija Kalili wa Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment