HATIMAYE ‘filamu’ ya ujio wa aliyekuwa Kocha wa timu ya soka ya 
Tanzania, Taifa Stars, Marcio Maximo kujiunga na Yanga imefikia tamati 
jana, baada ya uongozi wa klabu hiyo kukiri Mbrazil huyo kutokuja na 
kuwa wanatarajia kumtangaza kocha mpya wiki ijayo.
  Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesiga 
Selestine alisema, kocha huyo atatoka katika nchi zilizopo Amerika 
Kusini au Ulaya.
Alisema, uongozi ulipitia maombi ya makocha 25 waliotuma wasifu zao 
kwa ajili ya kutaka kibarua katika klabu hiyo, ambapo wamewachuja na 
kubaki watano.
  Akizungumzia suala la Maximo, katibu huyo alisema, wameamua kuachana 
naye kwa vile bado ana mkataba na klabu yake ya Democrata FC ya Rio de 
Janeiro, Brazil huku pia akipata ofa za kufundisha timu mbalimbali za 
taifa, ikiwemo Rwanda ‘Amavubi’.
“Kwa sababu hizo, isingekuwa rahisi kumchukua Maximo kufundisha Yanga,
 kwa mantiki hiyo tumeshafanyia mchujo maombi na kubaki makocha watano, 
ambapo mmojawapo ndiye atakayekuja kuinoa Yanga,” alisema.
  Hivi karibuni, Yanga ilitangaza ujio wa Maximo nchini kwa ajili ya 
kurithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Papic ‘Clinton’ ambaye alitupiwa 
virago miezi michache kabla ya kumaliza mkataba wake, kutokana na 
kushindwa kuiletea mafanikio timu hiyo.
Hata hivyo, kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele, ujio wa Maximo 
ulibaki kuwa ‘kiza kinene’ huku uongozi ukitoa ahadi kila kukicha, kabla
 ya jana kukiri kuwa hawezi kuja tena.
  Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi yake 
kwenye Uwanja wa Kaunda chini ya Kocha msaidizi, Fred Felix Minziro, 
ikiwa ni maandalizi ya michuano ya Kagame inayotarajiwa kuanza kutimua 
vumbi Julai 14.
No comments:
Post a Comment