TIMU ya soka ya Tanzania, Kili Taifa Stars, jana ilivuna ushindi
 wake wa kwanza katika hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya kucheza 
fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, nchini Brazil kwa kuifunga Gambia 
mabao 2-1.
  Wakitoka kufungwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza dhidi ya Ivory 
Coast wiki moja iliyopita mjini Abidjan, jana Stars waliwapa faraja 
wapenzi na mashabiki wa soka nchini.
Licha ya Stars kuanza kwa nguvu mechi hiyo kwa lengo la kushinda mbele
 ya mashabiki wake kupoza machunu ya kufungwa mechi ya kwanza, kwa 
mshangao wa wengi, dakika ya saba waliruhusu bao, likifungwa kwa kichwa 
  na Momodou Ceesay kutokana na krosi ya Saihou Gassama.
  Stars walipambana kusawazisha bao hilo kwa kufanya mashambulizi, 
Mwinyi Kazimoto alikosa nafasi kadhaa za kufunga kama Amir Maftah 
aliyeshindwa kufunga dakika ya 32, pale mkwaju wake wa faulo ulipodakwa.
  Kipindi cha pili kilianza kwa ushindani mkubwa kwani wakati Stars 
ikisaka bao la kusawazisha, huku wakipoteza nafasi kadhaa za kufunga, 
Gambia walijitutumua kulinda huku wakishambulia kwa kushtukiza.
Dakika ya 60, Shomari Kapombe aliifungia Stars bao la kusawazisha kwa 
kichwa cha kuparaza, hivyo nderemo na vifijo vya mashabiki kuuhanikiza 
Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
  Kapombe alifunga bao hilo kutokana na juhudi kubwa ya Erasto Nyoni, aliyetoa pasi ya mwisho kwa mfungaji.
  Baada ya bao hilo, Stars walionekana kupata nguvu zaidi za kupanga mashambulizi.
  Dakika ya 75, Kazimoto alifumua shuti ambalo lilichezwa na kipa wa Gambia, Christopher Alen.
  Dakika ya 78, Mrisho Ngassa nae alifumua shuti ambalo pia 
lilipanguliwa na kipa huyo aliyefanya kazi kubwa ya kupunguza idadi ya 
mabao ya Stars kwa uhodari wake langoni.
Wakati ikionekana pengine mechi hiyo ingeisha kwa sare ya bao 1-1, 
dakika ya 83, Nyoni akaifungia Stars bao la ushindi kwa penalti baada ya
 mmoja wa mabeki wa Gambia kuushika mpira ndani ya maguu 12.
  Kwa ushindi huo, Stars sasa ina pointi tatu, huku Gambia wakibaki na 
pointi moja waliyovuna kwa Morocco katika mechi ya wiki iliyopita, 
wakitoka sare ya 1-1.
Mechi za kampeni hiyo zitaendelea Machi 21, mwakani kwa Stars kuwakaribisha Morocco, huku Gambia wakiwa wageni wa Ivory Coast.
  Stars: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah, Erasto Nyoni, Kevin 
Yondani, Mrisho Ngassa, Frank Domayo, Mbawana Samata, Mwinyi Kazimoto, 
John Bocco na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
  Gambia: Christopher Alen, Ousman Koli, Pasaikou Kujabu, Abdou Koli, 
Abdou Jammek, Momodou Ceesay, Pamodou Jagne, Mustaph Jarju, Demba 
Savage, Saihou Gassama, Yankuba Ceesay na Momodou Danso.
No comments:
Post a Comment