WATU tisa wamefariki papo hapo na wengine 20 kujeruhiwa katika
ajali iliyohusisha magari mawili eneo la Ntangano Ijombe Mbeya Vijijini
barabara ya Mbeya- Kyela.
Ajali hiyo imelihusisha roli lenye namba za usajili T.658 ASJ
lililokuwa na tela namba T.150 ASN iliyokuwa ikitokea mpakani mwa
Tanzania na Malawi (Kasumulu) pamoja na Costa yenye namba T.886 BDZ
iliyokuwa ikitokea jijini Mbeya kuelekea wilayani Kyela.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya Dk. Eliuter Samky amethibitisha
kupokea maiti tisa wakiwamo wanawake watatu pamoja na majeruhi 20 na
kusema kuwa mara baada ya majeruhi kufikishwa hospitalini hapo watu
wanne walipoteza maisha wakiwa katika harakati za kupatiwa matibabu.
“Ni kweli tumepokea idadi hiyo ya maiti lakini kati ya majeruhi 20
tuliowapokea tayari wanne wamepoteza maisha na wengine watatu wako
katika hali mbaya na wamelazwa katika chumba cha wagonjwa wa dharura,”
alisema Dk. Samky.
Aidha alisema majeruhi wengine 16 wanaendelea kupata matibabu
hospitalini hapo kwa kuchukuliwa vipimo wakati watakaokuwa wamepata
matibabu wataruhusiwa kwenda nyumbani.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, ilitokea majira ya saa nane
kasoro robo mchana ambapo roli likiwa katika mwendo kasi likijaribu
kukata kona kali lilizidiwa hivyo tela kuigonga Costa na kusababisha
ajali hiyo.
Akizungumza katika eneo la tukio Safari Samson shuhuda wa ajali hiyo
aliwaambia waandishi wa habari kuwa dereva wa Costa aliyemtambua kwa
jina moja la Mwasa mkazi wa Ilomba jijini Mbeya ni mmoja wa watu
waliofariki papo hapo.
“Nimefika eneo hili mapema sana kwani Costa hii ni ya ndugu yangu
baada ya kupigiwa simu kuwa gari ya ndugu yangu imepata ajili,
nilishuhudia maiti nane ikiwamo ya dereva wa Costa zikitolewa eneo hili
na kwenye roli tumetoa maiti moja ambapo dereva wa roli amekimbia,”
alisema.
Naye utingo wa roli lililopata ajali, Christopher Mgaya (32), mkazi wa
Dar es Salaam alisema kuwa walikuwa wakitokea mpakani kuelekea Dar es
Salaam wakishuka katika mtelemko kwenye kona aliona Costa ikipandisha
mlima ghafla tela lilicheza ndipo mwenye Costa akajibamiza kwenye tela
na kusababisha ajali hiyo.
“Kwenye roli tulikuwa watatu, mimi, dereva ninayemtambua kwa jina moja
tu la Peter pamoja na abiria mmoja ambaye tulimpakia akiwa na mzigo
wake wa maparachichi na machungwa hata hivyo alifariki, lakini dereva
amenieleza kuwa shingo inamuuma sana hivyo ametangulia hospitali.
No comments:
Post a Comment