Friday, June 22, 2012

Filamu ya Maximo Yanga yafika tamati

HATIMAYE ‘filamu’ ya ujio wa aliyekuwa Kocha wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Marcio Maximo kujiunga na Yanga imefikia tamati jana, baada ya uongozi wa klabu hiyo kukiri Mbrazil huyo kutokuja na kuwa wanatarajia kumtangaza kocha mpya wiki ijayo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesiga Selestine alisema, kocha huyo atatoka katika nchi zilizopo Amerika Kusini au Ulaya.

Alisema, uongozi ulipitia maombi ya makocha 25 waliotuma wasifu zao kwa ajili ya kutaka kibarua katika klabu hiyo, ambapo wamewachuja na kubaki watano.
Akizungumzia suala la Maximo, katibu huyo alisema, wameamua kuachana naye kwa vile bado ana mkataba na klabu yake ya Democrata FC ya Rio de Janeiro, Brazil huku pia akipata ofa za kufundisha timu mbalimbali za taifa, ikiwemo Rwanda ‘Amavubi’.

“Kwa sababu hizo, isingekuwa rahisi kumchukua Maximo kufundisha Yanga, kwa mantiki hiyo tumeshafanyia mchujo maombi na kubaki makocha watano, ambapo mmojawapo ndiye atakayekuja kuinoa Yanga,” alisema.
Hivi karibuni, Yanga ilitangaza ujio wa Maximo nchini kwa ajili ya kurithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Papic ‘Clinton’ ambaye alitupiwa virago miezi michache kabla ya kumaliza mkataba wake, kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio timu hiyo.

Hata hivyo, kadiri siku zilivyokuwa zikisonga mbele, ujio wa Maximo ulibaki kuwa ‘kiza kinene’ huku uongozi ukitoa ahadi kila kukicha, kabla ya jana kukiri kuwa hawezi kuja tena.
Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi yake kwenye Uwanja wa Kaunda chini ya Kocha msaidizi, Fred Felix Minziro, ikiwa ni maandalizi ya michuano ya Kagame inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 14.

Wednesday, June 20, 2012

Rais amteua wakili wa Lulu kuwa Jaji

RAIS Jakaya Kikwete amemwapisha kuwa Jaji wakili wa kujitegemea, Joaquine De-Mello ambaye alikuwa akimtetea msanii wa filamu Elizabeth Michael (Lulu)  anayetuhumiwa kwa mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Wakili huyo, ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King ya mwaka 2012 na ambaye alikuwa pia alikuwa mmoja wa makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) ni miongoni mwa majaji 10 walioapishwa jana na Rais Kikwete, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
De-Mello ni miongoni mwa mawakili wanne waliojitokeza Aprili mwaka huu kumtetea Lulu katika kesi hiyo ya mauaji inayomtuhumu kumuua usiku wa kuamkia Aprili 7, mwaka huu.

Mawakili wengine wanaomtetea Lulu ambaye umri wake umekuwa na utata ni Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe.

Akizungumza kwenye viwanja vya Ikulu, De-Mello alisema baada ya kuteuliwa kuwa Jaji, sasa atafanya kazi hiyo na moja ya mikakati yake ni kukabiliana na changamoto za wingi wa kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Majaji wengine walioapishwa jana na Rais Kikwete ni Francis Mutungi, John Mgeta, Patricia Fikirini, Sam Rumanyika, Salvatory Bongole, Jerald Alex, Mathew Mwaim, Jacob Mwambegele na Latifa Mansook.
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman alisema amefurahi kuteuliwa kwa majaji hao na anawafahamu kuwa wote ni wazoefu na watatekeleza kazi zao kikamilifu.

“Wote ni wazoefu. Ukiangalia utaona kuwa sita walikuwa wakifanya kazi mahakamani (Mahakama Kuu na Rufani), wawili mawakili wa kujitegemea na wawili pia mawakili wa Serikali,” alisema Jaji Othman.
Alisema majaji hao wote kabla ya kupangiwa kazi rasmi itabidi waanze kufanya kazi ya kukabiliana na kesi zaidi ya 2,200 zilizopo katika Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi.

Uteuzi wa majaji hao 10, alisema unaifanya Mahakama Kuu sasa kuwa nao 69 tofauti na wale 16 wanaounda Mahakama ya Rufani.
Othman alisema pamoja na uteuzi huo wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kulundikana kwa kesi nyingi kuliko uwezo wao.
“Walioteuliwa watasaidia lakini ukweli ni kwamba bado tunakabiliwa na upungufu wa majaji. Kesi ni nyingi,” alisema Othman.

Hakuweza kueleza mara moja idadi kamili ya majaji inayotakiwa ili kukidhi mahitaji lakini akasema kuwa Serikali imeliona hilo na imekuwa ikilifanyia kazi hatua kwa hatua.

Licha ya upungufu wa majaji, Jaji Othman alisema wanakabiliwa na tatizo la kutumia teknolojia ya zamani ya kusikiliza na kuandika tofauti na maendeleo ya sasa ambayo yanahitaji kurekodi.
“Mfumo huu wa kutumia teknolojia ya kisasa pia ungeweza kuharakisha kesi,” alisema Jaji Othman lakini akasema Kitengo cha Biashara tayari kimeanza kuifanyia kazi teknolojia ya kisasa.

Kwa kutumia teknolojia hiyo, alisema mtu anaweza kutumia simu yake ya mkononi kujua siku ya kesi yake na hata kuperuzi kwenye mtandao kupata hukumu pamoja na mwenendo wa kesi yake.
Alisema wanatarajia kwenda hatua kwa hatua ili kuhakikisha teknolojia hiyo ya kurahisisha kazi za mahakama inaenea idara zote za Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Majaji wengine wapya nao walisema kwenye mahojiano na waandishi wa habari kwamba moja ya changamoto ni kufanya kazi katika mazingira magumu na wingi wa kesi zilizolundikana katika mahakama hiyo.
Jaji Mutungi alisema yeye anaamini kiu kubwa ya Watanzania ni kupatiwa haki na kwamba haki hiyo inapocheleweshwa pia ni tatizo jingine.

Ili kuhakikisha anawatekelezea Watanzania haki zao, Mutungi alisema atajitahidi kufanya kazi kwa bidii na kumaliza kesi nyingi kwa haraka.

Kwa upande wake, Jaji Mgeta alisema pamoja na wingi wa kesi kazi kubwa wanayopaswa kuifanya ni kuwa waadilifu na watenda haki.

Alikiri kwamba Tanzania wako nyuma katika teknolojia ya kuendesha kesi lakini akasema hilo halipaswi kuwa ni jambo ambalo litawafanya warudi nyuma na kutotekeleza wajibu wao kikamilifu.

Tuesday, June 19, 2012

TASWIRA ZA JOHN MNYIKA AKITOLEWA BUNGENI LEO


Mbunge wa jimbo la Ubungo John Mnyika akitoka nje ya viwanja vya  Bunge la Tanzania leo mjini Dodoma baada ya kukataa kufuta kauli ya kumdhalilisha Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania kuwa dhaifu. Mbunge huyo alitoa kauli hiyo wakati akichangia Bajeti ya serikali ya mwaka 2012/13 katika mkutano unaoendelea.

Mbunge wa Jimbo la Ubungo John Mnyika akiteta na Mbunge wa jimbo la Wawi Hamad Rashid Mohamed (kushoto) na Mbunge wa Bariadi Mashariki John Cheyo  mara baada ya kuondolewa Bungeni leo mjini Dodoma baada ya kukataa kufuta kauli ya kumdhalilisha Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania kuwa dhaifu. Mbunge huyo alitoa kauli hiyo wakati akichangia Bajeti ya serikali ya mwaka 2012/13 katika mkutano unaoendelea.
Mbunge wa jimbo la Ubungo John Mnyika akitoka katika ukumbi wa Bunge la Tanzania leo mjini Dodoma baada ya kukataa kufuta kauli ya kumdhalilisha Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania kuwa dhaifu. Mbunge huyo alitoa kauli hiyo wakati akichangia Bajeti ya serikali ya mwaka 2012/13 katika mkutano unaoendelea.
(Picha na Tiganya Vincent- MAELEZO- Dodoma)

DIAMOND ANUNUA GARI JIPYA LA TSH MIL. 60

Staa wa muziki wa kizazi kipya  Bongo, Naseeb Abdul  ‘Diamond  Platinumz’ amevuta mkoko wa Kijanja  wenye thamani ya ‘mkwanja wa Kibongo Milioni  60 keshi.
Akizungumza na Teentz.com  muda mfupi  baada ya  kupokea  ‘dinga’ hiyo aina ya Land Cruiser Prado TX  kutoka kwa wakala aliyekuwa akishughulikiwa  mpango mzima  wa  kuingia kwake  hapa  Bongo, Diamond  alifunguka kuwa alikuwa na mpango wa kuvuta  mkoko ‘dizaini’ hiyo kitambo lakini  kuna mambo kadhaa yakawa …
“Nashukuru Mungu kuwa  mpango wangu umetimia, nilipanga hivi kitambo lakini kuna baadhi ya mambo yalichelewesha hatua hiyo, najua watu watasenama mengi kuhusu  hili lakini ukweli ni kuwa  huu ni mchuma wangu” alisema Diamond.



Monday, June 18, 2012

LOVE ME OR LOVE ME NOT IPO SOKONI


Filam inayokwenda kwa jina la LOVE ME OR LOVE ME NOT iliyotayarishwa na Ndauka intertaiment chini ya usimamizi wa Director wa kampuni hiyo Rose Ndauka imeindia sokoni wiki mbili zilizopita. 

Filam hiyo imeonekana kufanya vizuri tangu kuingia sokoni kutokana na ubora wa kazi iliyofanyika katika uandaaji wa filam hiyo.

 

 Akizungumza na Ndauka promotion blog, Rose amesema wapenzi wake wategemee kazi nzuri zinazokuja baada ya love me or love me not ikiwepo  filam za action ambazo anaziandaa kwa ubora wa hali ya juu.



Msomi UDSM awa Miss Kigamboni


Miss Kigamboni 2012, Edda Sylvester (katikati) akiwa na mshindi wa pili Agnes Goodluck (kushoto) na mshindi wa tatu Elizabeth Boniphace mara baada ya kutangwazwa washindi.
Edda Silyvester, 21, ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani alitwaa taji la Miss Kigamboni katika shindano lililofanyika kwenye ukumbi wa Navy Beach usiku wa kuamkia jana, na kuingia hatua ya Kanda akiongoza wasichana wengine wanne.
Jaji mkuu wa shindano hilo, Benny Kisaka, alitangaza kuwa badala ya warembo watatu, watachukua warembo washindi watano wa kwanza miongoni mwa washiriki tisa kuingia shindano la Kanda ya Temeke baadaye mwaka huu.
Kutokana na ushindi huo Edda alizawadiwa Sh.500,000 taslimu na mgeni rasmi katika shindano hilo, diwani wa Kata ya Kigamboni, Dotto Msawa.Nafasi ya pili katika shindano hilo lililopambwa na burudani safi kutoka bendi ya FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma' ilichukuliwa na Agnes Goodluck ambaye alipata zawadi ya Sh.350,000.
Elizabeth Boniface alichaguliwa kuwa mshindi wa tatu na kupata zawadi ya Sh.300,000. Esther Albert na Khadija Kombo walishika nafasi za nne na tano na kila mmoja alipata zawadi ya Sh.200,000.
Warembo wengine walioshiriki shindano hilo walikuwa ni Sophia Martin, Rosemary Peter, Doreen Kweka na Linnah David waliopewa kifuta jasho cha Sh.150,000 kila mmoja.
Wakati huo huo, Matlda Martine alitwaa taji la Miss Dar City Centre katika shindano lingine lililofanyika jijini juzi usiku pia.

Diamond kutumbuiza Miss Arusha

Msanii Diamond
Aidha aliwataja watumbuizaji kuwa ni pamoja na msanii Diamond atakayebeba onyesho zima kwa upande wa burudani ambaye atasindikizwa na kikundi cha ngoma na kudansi cha Boda2Boda cha mkoani hapa pamoja na msichana Sister P wa mkoa wa Arusha ambaye ni mwimbaji wa miondoko ya reggae.

Alisema kuwa jumla ya warembo 20 kutoka vitongoji vinne vya mkoa wa Arusha wameingiaa kambini kujiandaa na shindano hilo. Alisema warembo hao ni washindi wa kutoka vitongoji vya Miss Arusha City Centre, Njiro, Sakina na Monduli.

"Kwa kweli sio kama najisifu ila warembo wetu ni wazuri na nina imani watashinda maana wana upeo, elimu ya kutosha na maadalizi ni mazuri.

"Kingine kikubwa mwaka huu ni kwamba mashindano haya yatakuwa tofauti sana kwani tumejipanga vilivyo na hatutaki kufanya makosa.

Kwanini kila siku taji liende Dar na Mwanza tu, safari hii nitahakikisha linakuja Arusha," alisema Mwandago.

Aliwataja wadhamini wa shindano hilo kuwa ni TBL, Dodoma Wine, Tanzanite One, Mogaben Priters, Libeneke la Kaskazini blog na Arusha Traveling Lodge ambao ndio wametoa kambi ya warembo.
 

Mhariri Jambo Leo afariki

KWA mara nyingine tasnia ya habari nchini imepata pigo la kuondokewa na Mhariri Mkuu wa gazeti la kila siku la Jambo Leo, Willy Edward (38), aliyefariki ghafla usiku wa kuamkia jana akiwa mjini Morogoro.
Willy pamoja na wahariri wenzake wa vyombo mbalimbali vya habari, walikuwa mkoani humo, kuhudhuria semina ya siku moja iliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kuhusu sensa ya watu na makazi.
Taarifa za kifo chake zilitolewa na mhariri mwenzake wa gazeti la Mtanzania, Kulwa Karedia, ambaye alikuwa naye kabla ya kufikwa umauti, akisema kuwa alikuwa ni mzima wa afya, na kwamba aliwaaga anakwenda kuwaona watoto wake ambapo alikaa huko mpaka saa 6:30 usiku.
Alisema muda wa kurudi hotelini alikokuwa amefikia ulipofika, Willy alimwita dereva wa pikipiki ili amchukue, lakini usafiri huo ulipofika hakuweza kuupanda kwani alipotoka nje na kutembea kwa hatua chache alianguka.
Karedia aliongeza kuwa, ndugu zake walimkimbiza hospitalini na baada ya vipimo vya daktari, ikabainika kuwa alikwishafariki dunia.
 
Kaka wa marehemu azungumza
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kaka wa marehemu, Denis Ongiri, alisema wanatarajia kuzika mjini Mugumu wilayani Serengeti, Mara.
Alisema kwa sasa msiba upo nyumbani kwa kaka yao eneo la Mburahati NHC na kwamba taratibu za kusafirisha mwili kwa ajili ya mazishi zitatolewa baada ya ndugu kukutana na kutoa uamuzi wa pamoja.
“Suala hili limekuwa la ghafla sana, ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba tutaenda kumzika wilayani Serengeti katika mji wa Mugumu, tunaomba ushirikiano wa watu wote katika hili kuanzia sasa mpaka safari yake ya mwisho,” alisema Ongiri.
Mwili wa marehemu Willy, ulihamishwa toka Hospitali ya Mkoa Morogoro jana na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam ambako utahifadhiwa.
Gari lililobeba mwili huo, liliwasili Muhimbili jana majira ya saa 11 jioni likiwa na wanafamilia na wanahabari kadhaa kisha mwili kushushwa na kuingizwa chumba cha kuhifadhia maiti.
Wakati wa kupokea mwili huo, watu mbalimbali wakiwemo wanahabari, walishindwa kujizuia na hivyo kuangua vilio wasiamini kile walichokuwa wakikishuhudia.

Historia yake
Willy Edward Daniel Ogunde, alizaliwa Machi 7, 1974 katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, na kusoma Shule ya Msingi Mapinduzi mwaka 1983-89. Elimu ya sekondari aliipata katika shule ya Serengeti mwaka 1990-93 na kuendelea na kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Musoma.
Mwaka 1996 alijiunga na kampuni ya uchapishaji wa magazeti ya Business Times Ltd (BTL) akiwa mwandishi wa gazeti likiitwa Majira Jioni wakati huo.
Akiwa na kampuni hiyo, alipata mafunzo mafupi ya kikazi yakiwemo ya kompyuta na ya uandishi wa habari.
Mwaka 1998 alihamishwa kitengo kutoka kwenye gazeti la Majira Jioni kwenda kwenye gazeti jipya la Dar Leo na kuwa mwandishi wa habari wa gazeti hilo, lakini pia akishikilia nafasi ambazo alikuwa akizitumikia kwenye gazeti la Majira Jioni.
Alifanikiwa kuaminika kutokana na uwezo wake kazini na hivyo alipanda daraja na kuwa mhariri wa gazeti la 
Dar Leo kuanzia mwaka 2002 hadi 2005.
Kipindi cha mwaka 2006 hadi 2007 alikuwa akitumikia nafasi ya mhariri msaidizi wa michezo wa gazeti la Majira na baadaye mwaka huo akawa mhariri wa michezo wa gazeti hilo.
Mwaka 2006 hadi 2007 alipata cheti cha elimu ya uandishi wa habari katika Chuo cha Ceylon (CSJ).
Amesafiri nchi mbalimbali duniani katika kuripoti habari za michezo na burudani, ikiwemo Afrika Kusini mwaka 2003 hadi 2006 kwenye mashindano ya Big Brother Africa.
Pia mwaka 2007, 2008 na 2009 alikwenda Kenya, Senegal na Uingereza kuripoti habari za michezo kupitia Super Sport.

Mei mwaka huu, alisafiri kwenda nchini Uturuki kwenye kongamano la wadau wa masuala ya mawasiliano, ambako alikuwa kiongozi wa wahariri waliotoka Tanzania na kutoa mada iliyohusu mwenendo wa vyombo vya habari nchini Tanzania.
Nje ya kazi ya uandishi wa habari, mwaka 2008 na 2009 alifanya kazi katika kampuni ya matangazo ya ZK akiwa Ofisa Habari na Uhusiano.
Miongoni mwa vyombo vya habari ambavyo aliwahi kufanya kazi enzi za uhai wake ni pamoja na kampuni ya New Habari ambayo aliitumikia mwaka 2007 na 2008 akiwa mhariri msaidizi wa gazeti la Bingwa.
Hatimaye mwaka 2008 alikuwa mhariri mkuu wa gazeti la Bingwa kabla hajaacha kazi katika kampuni hiyo na kujiunga na ZK.
Mwaka 2010 alijiunga na gazeti la Jambo Leo, akiwa mhariri wa habari na kuanzia mwaka jana hadi mauti yalipomkuta alikuwa mhariri mkuu wa gazeti hilo.
Marehemu ameacha mke na watoto watatu, mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi. Amina
CHANZO CHA HABARI:http://www.freemedia.co.tz/daima

Umasikini chanzo cha watoto wa mitaani’

WIZARA ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, imesema kuwa umasikini uliokithiri miongoni mwa jamii ni moja ya chanzo cha wimbi kubwa la watoto wa mitaani.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, Elisante ole Gabriel, alitoa kauli hiyo juzi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyoandaliwa na Shirika la Hope for the Children Organization.

Akizungumza kwa niaba yake, ofisa mwandamizi wa idara hiyo, Focas Kapinga, alisema jamii inapaswa kutambua kuwa jukumu la kuwalea watoto hao ni la Watanzania wote.
Kwamba umasikini umekuwa ukichangia hali hiyo ya watoto wa mitaani kutokana na baadhi ya wazazi kushindwa kuzihudumia familia zao ipasavyo, matokeo yake watoto huamua kukimbilia mitaani kwa matumaini ya kupata maisha bora.

Kapinga alisema kuvunjika kwa ndoa kumekuwa kukisababisha familia kushindwa kukidhi mahitaji muhimu kwa watoto, kama vile elimu, chakula, mavazi hali inayowalazimisha kuondoka majumbani kwao.
Alibainisha kuwa, wizara hiyo ndiyo yenye jukumu la maendeleo ya vijana, wakiwemo watoto, na kwamba dhamira yao ni kukabiliana na mambo yanayosababisha watoto kukimbilia mitaani.
“Wizara imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika ya kimataifa kama vile UNICEF, ILO, UNEPA, UNDP na ya watu binafsi yaliyoko nchini na taasisi za dini katika kutimiza azma yake,” alisema.
Kapinga alibainisha kuwa, jitihada hizo ni pamoja na utoaji wa elimu ya ujasiriamali, stadi za maisha na mikopo kwa vijana yenye masharti nafuu.
Awali Mkurugenzi wa Hope for the Children Organization, Joyce Mang’o, alisema pamoja na mipango mingi ya serikali, lakini bado imekuwa ikitoa mchango hafifu wa kupambana na tatizo hilo.
Alisema sheria zilizopo hazilengi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa asasi na watoto pia, jambo linalosababisha asasi kuwa na utendaji hafifu usiokidhi haja na matakwa kwa wahusika.

Sunday, June 17, 2012

LISA NDIYE MISS TANZANIA 2012

KIMWANA Lisa Jensen usiku huu ameibuka kinara katika shindano maalum la kumsaka mwakilishi wa Tanzania katka shindano la Miss World mwaka huu, lililofanyika kwenye ukumbi wa 327, Mikocheni, Dar es Salaam.
 
Shindano hilo, lililoshirikisha washiriki wa zamani wa Miss Tanzania ambao hawajawahi kushinda, dalili za Lisa kushinda zilionekana tangu mwanzo, kutokana na kuwafunika washiriki ‘ile mbayaaa’ washiriki wenzake tisa.
Shindano hilo, lilianzia kwa warembo kucheza shoo ya ufunguzi kama ilivyo ada ya mashindano ya Miss Tanzania, baadaye wakapita na vazi la ubunifu, ufukweni na kumalizia na vazi la jioni, ambako kote Miss Mara wa 2006 alifunika mbaya.
Jaji Mkuu wakitangaza top 5
 
Aliyemfuatia Lisa ni Hamisa Hassan kutoka Kinondoni, wakati mshindi wa tatu alikuwa ni Pendo Laiser Miss Arusha 2008 na wengine walioingia tano bora ni Stella Mbuge na Jennifer Kakolaki.
Washiriki wengine ni Glorybayanca Mayowa, Queen Issa, Christine William, Mwajabu Juma na Neema Saleh.
 
Shindano hili, linafanyika kufuatia kalenda ya mashindano ya Miss Tanzania kubadilika na washindi wa mashindano ya mwaka huu ngazi ya awali watashiriki katika shindano la Miss Tanzania baadaye mwaka huu, kumpata mwakilishi wa Miss World mwakani.

Warembo shoo ya ufunguzi

Lisa akipongezwa na Salha, Miss Tanzania 2011 baada ya kuvikwa taji

Majaji wakipiga hesabu

Waalikwa
Sura za furaha
Glory na rafiki zake
Waalikwa
Top three
Mwaaa! hongera mama, Salha akimvisha taji Lissa

Mrusi amkimbia Matumla Moshi

BONDIA wa Urusi, Vitaly Shemetov maarufu kama ‘Siberian Tiger’ ameingia mitini yeye na kocha wake kuja nchini kupambana na mkongwe, Rashid Matumla ‘Snake Man’.

Shemetov na kocha wake, walitumiwa tiketi za ndege ya shirika la Kirusi la Aeroflot, ili kuja nchini kwa ajili ya pambano hilo litakalorindima Juni 24 mjini Moshi, wakati wa Mbio za Mount Kilimanjaro.
Kwa mujibu Rais wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa Afrika (IBF), Onesmo Ngowi, hii ni mara ya kwanza kwa pambano la kimataifa lilioandaliwa kwa fedha nyingi, kutofanyika baada ya bondia huyo kuingia mitini kwa madai ya woga.

Ngowi alisema, Matumla ana rekodi ambayo hadi sasa hakuna bondia yeyote wa Kitanzania aliyeweza kuifikia.
“Matumla ameshawahi kuwa bingwa wa Taifa, Afrika Mashariki na Kati, Bara la Afrika, mabara na dunia aliyetambuliwa na Umoja wa Ngumi Duniani (WBU),” alisema Ngowi na kuongeza; akiwa chini ya DJB Promotions, bondia huyo ambaye kwa sasa ndiye Kamishna wa TPBC kanda maalumu ya Dar es Salaam, alionyesha alionesha kiwango cha hali ya juu.

MAGAZETI YA LEO JUMAPILI

MAGAZETI YA LEO JUMAPILI HAPA....












Saturday, June 16, 2012

EDDA SYLVESTER ATWAA TAJI LA MISS KIGAMBONI 2012

 Redds Miss Kigamboni City  2012 , Edda Sylvester (katikati) akiwa na washindi wenzake, mshindi wa pili Agnes Goodluck (kushoto) na mshindi wa tatu Elizabeth Boniphace, baada ya kutangwazwa washindi. katika shindano lililofanyika usiku wa kuamkia leo kwenye Ukumbi wa Nev Beach, Kigamboni. Edda ameibika kidedea baada ya kuwamwaga warembo wenzake  9 katika shindano hilo. Picha zote na Mroki Mroki
 Warembo walioshiriki katika shindano hilo, wakicheza shoo ya pamoja ya ufunguzi jukwaani.
 Wanenguaji wa Bendi ya Fm Academia, wakiongozwa na Qeen Suzy,  wakishambulia jukwaa katika kusindikiza shindano hilo.
 Warembo walioingia hatua ya tano bora ya Miss Kigamboni 2012, kutoka kulia ni  Elizabeth Boniface, Ester Albert, Edna Sylvester, Hadija Kombo na Agnes Goodluck, wakipozi kwa picha jukwaani baada ya kutangazwa kuvuka nafasi hiyo na kupata tiketi ya kushiriki shindano la Miss Temeke 2012 baadaye mwaka huu.
 Mrembo Edda Sylvester (21) akipita jukwaani na kivazi cha ufukweni wakati wa shindano la kumsakaka Miss kigamboni City  lililofanyika katika Ukumbi wa Navy Beach Kigamboni jijini Dar es usiku wa kuamkia leo.  
Mrembo, akipita jukwaani na vazi la Ufukweni, wakati wa shindano la kumsakaka Miss kigamboni City  lililofanyika katika Ukumbi wa Navy Kigamboni jijini Dar es salaam.

England yapata ushindi wa kusisimua


England na Sweden
England imeiondoa Sweden katika mashindano ya Euro 2012
Danny Welbeck aliweza kuandikisha bao la ushindi la England dhidi ya Sweden, katika mechi ya kusisimua ya kundi D.
England iliweza kutangulia kwa bao la kwanza wakati Andy Caroll alipofunga kwa kichwa, baada ya kuletewa mpira wa juujuu kutoka kwa Steven Gerrard.

Lakini mlinzi Olof Mellberg aliweza kufunga bao la kusawazisha, na baadaye kupata la pili kwa kichwa na kuiwezesha Sweden kuongoza kwa mabao 2-1.

Mchezaji wa zamu Theo Walcott kupitia mkwaju kutoka yadi 25 aliiwezesha England kusawazisha, na kisha baadaye alipompigia mpira Welbeck, akafanikiwa kufunga bao la tatu na la ushindi, na kuhakikisha Sweden wanaelekea nyumbani baada ya kuwaondoa katika mashindano ya mwaka huu ya Euro 2012.
Huu ndio ushindi mkubwa zaidi wa England dhidi ya timu ya Sweden, na mara tu baada ya Carroll kuwawezesha kuongoza, England haikuona tena kitisho kikubwa mno cha kulemewa katika mechi hiyo ya Ijumaa.

Pengine onyo la nahodha Steven Gerrard kabla ya mechi katika kuhakikisha mshambulizi Zlatan Ibrahimovic asipate nafasi za kufunga labda ziliweza kuisaidia England kuepuka kushindwa.
Lakini kwa kumzuia Ibrahimovic, pengine ndio maana mchezaji mwenzake Melberg alipata bao la pili la Sweden kwa urahisi kwa kuwa England hawakumzuia kikamilifu.
Meneja wa England Roy Hodgson kisha aliamua kumtumia Walcott, na bila shaka mchezaji huyo alibadilisha mchezo.

Rachael Ndauka



Rachael Ndauka Katika picha.

Friday, June 15, 2012

SAUDA MWILIMA AJIFUNGUA

MTANGAZAJI wa Kipindi cha Bongo Beats cha StarTV, Sauda Mwilima (pichani) amepata pigo baada ya mtoto aliyejifungua Juni 12, mwaka huu kuwa siyo riziki yake.

Chanzo chetu cha habari ambacho ni rafiki wa karibu wa mtangazi huyo, kikizungumza na Ijumaa kilisema Sauda alipata uchungu wa kujifungua mishale ya jioni.

Kiliongeza kuwa, baada ya kupatwa na hali hiyo alikimbizwa katika Hospitali ya Dk. Mvungi iliyopo Kinondoni B jijini Dar ambapo iligundulika kwamba mtoto alifia tumboni.

“Inawezekana mtoto alifia tumboni wakiwa njiani kumleta hapa,” alisema mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo aliyeomba hifadhi ya jina.
Sauda alipotafutwa kwa njia simu ili kusikia kauli yake kuhusiana na masahibu yaliyomkuta hakuweza kupatikana lakini mumewe, Kauli Juma ambaye yuko Afrika Kusini alikiri kutokea tatizo hilo.

KUNA TISHIO LA LULU KUUAWA?

HATIMAYE siri ya kumwekea ulinzi mkali Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambaye anakabiliwa na mashitaka ya kifo cha Steven Kanumba imebainika, Ijumaa lina cha kushika mkononi.

Siri hiyo ilitobolewa Jumatatu iliyopita na askari polisi mmoja ambaye hakuwa tayari kuweka hadharani jina, aliyepewa kazi ya kukagua watu wanaoingia kwenye Jengo la Mahakama ya Kuu kwa ajili kusikiliza kesi ya msanii huyo iliyokuwa ikitoa maamuzi ya kujadili umri wa Lulu.
Afande huyo alimtilia shaka mmoja wa waandishi wa habari ambapo ilibidi ampekue sehemu mbalimbali za mwili licha ya kujieleza na kuonesha kitambulisho chake cha kazi.
“Kitambulisho kitu gani bwana, watu wanavitengeneza tu siku hizi, mihuri ya bandia kibao tunapokutilia shaka ni lazima tujiridhishe bwana,” alisema askari huyo huku akiendelea na zoezi la kumkagua paparazi huyo na mwandishi wetu akiwa pembeni.
Yafuatayo ni mazungumzo kati ya mwandishi wetu na askari huyo.
Mwandishi: “Hivi ni kwa nini kitoto kidogo kama hiki mnakiwekea ulinzi wa kutisha kuliko hata muuaji wa kutumia bunduki?”
Askari: “We acha tu, unajua hii kesi ni tofauti kidogo na nyingine, huu ulinzi si kama tunahisi huyu mtoto anaweza kututoroka, hilo halipo. Isipokuwa kuna taarifa kuwa kuna kundi la watu linataka kumdhuru na hata kumuua ndiyo maana tumekuwa tukizidisha ulinzi kila tunapoona kuna haja ya kufanya hivyo.”
Mwandishi: “Kundi hilo ni la akina nani?”
Askari: “Hiyo ni siri ya ndani, lakini sisi tunasema ole wake mtu yeyote atakayenaswa akiwa katika mpango wa kutaka kutekeleza mpango huo au atakayethubutu, yaani naapa atakiona kilichomtoa kanga manyoya.”

Mwandishi: “Mbona alipokwenda chooni alisindikizwa na kundi la askari wa kike na wa kiume, yaani mnahisi hao maadui wanaweza kutekeleza mpango huo hata chooni?”
Askari: “Nimekwambia lengo ni kuimarisha ulinzi, hatuwezi kulegeza ulinzi mahali popote na hivi ninavyokwambia hata ulinzi wa Gereza la Segerea umeongezwa kwa ajili yake, kuna askari wametolewa magereza mbalimbali wameongezwa.”

Mwandishi: “Kwa hiyo mnaamini kundi hilo linalotaka kutekeleza mpango huo lina nguvu kubwa kama nyinyi? Maana mnawatumia askari wenye kofia za chuma, nguo za kuzuia risasi na bunduki aina ya SMG zenye risasi 60, mnaona hazitoshi mnaiwekea ‘magazine’ ya ziada yenye risasi nyingine kama 60 na kuna bunduki zaidi ya 20.”

Askari: “Siku zote unapotaka kupambana na adui yako ni lazima ujikamilishe, huwezi kujua mwenzio amejiandaa vipi, cha msingi sisi tumejiandaa vya kutosha, si unaona huu msafara wa magari matatu na askari zaidi ya 30, tena wenye silaha unazoziona na nyingine huzioni umetoka Segerea kuja hapa kwa ajili ya mtu mmoja.
“Ni gharama kubwa kwa serikali maana kuna askari walitakiwa kwenda likizo lakini wamelipwa kwa ajili ya kusitishiwa likizo zao kwa sababu ya huyu Lulu,” alisema askari huyo.
Akaongeza: “Hali hii ilianza akiwa kituo cha polisi (Oysterbay), kabla Kanumba hajazikwa.
“Hawa watu wakaweka mkakati wa kumpeleka Lulu aliko Kanumba, serikali ikalijua hilo.”
                    Chanzo cha habari na Na Richard Bukos wa Gazeti la ijumaa

Tuesday, June 12, 2012

BASATA: WASANII JIPANGENI KUHIMILI USHINDANI WA KIMATAIFA

Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego akisisitiza jambo wakati akihitimisha mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya BASATA.Wengine kulia ni 

Mhandishi Joel Chacha kutoka malaka ya mawasiliano nchini (Tcra) na Kaimu Mratibu wa Jukwaa hilo Agnes Kimwaga.
Bw. Joel Chacha kutoka mamlaka ya mawasiliano nchini Tcra akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii iliyohusu 

Teknolojia ya Digital na Faida Zake Katika Sekta ya Sanaa na Wasanii.Kulia ni Katibu Mtendaji wa BASATA Bw. Materego.
Mdau kutoka Mlimani TV akiuliza maswali kuhusu mfumo wa Digitali.

Mmoja wa Wasanii aliyehudhuria mjadala huo akitoa ya moyoni kuhusu mchakato wa kuhama kutoka mfumo wa analogia kwenda ule wa Digitali na mchango wake kwenye Sanaa.
Sehemu ya wadau wa Sanaa waliohudhuria mjadala huo wakifuatilia kwa makini elimu iliyokuwa inatolewa.

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kujipanga kwa ajili ya kuhimili ushindani wa kimataifa kutokana na ujio wa mfumo wa digitali ambao utazifanya kazi zao kuonekana kimataifa.

Wito huo umetolewa wiki hii kwenye ukumbi wa BASATA na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Ghonche Materego wakati akihitimisha mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa uliohusu Teknolojia ya Digital na Faida Zake Katika Sekta ya Sanaa uliochokozwa na Mhandisi Joel Chacha kutoka mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (Tcra).

Alisema kuwa, mfumo wa digitali utaruhusu uwepo wa vituo vingi vya redio na runinga ambavyo vitakuwa na masafa ya kimataifa hivyo ni wazi wasanii wanatakiwa kujipanga katika kuandaa maudhui bora, ya kutosha na yenye mvuto kwa ajili ya kukidhi ongezeko hilo na zaidi ushindani wa kimataifa.

“Wasanii tujipange, fursa zinazokuja ni nyingi mno, zinahitaji maudhui ya kutosha, yenye ubora na yatakayoweza kuvifanya vyombo vya habari viweze kuhimili ushindani pia” alisisitiza Materego.
Aliongeza kuwa, moja ya eneo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wamiliki wa vyombo vya habari ni uhafifu wa maudhui ya kazi za Sanaa hivyo, wasanii hawana budi kuacha kulalamika na kujipanga kukabili changamoto hiyo.

Awali akiwasilisha mada hiyo,Mhandisi Chacha alisema kuwa, mfumo wa digitali utazalisha fursa nyingi katika sekta ya Sanaa lakini akasisitiza kuwa, uchangamfu wa Wasanii wetu ndiyo utawafanya wafaidi.

Alizitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na; ongezeko la ajira kwa Wasanii, ongezeko la vipindi, kukua kwa ushindani katika ubunifu na utengenezaji maudhui yenye ubora, Sanaa za Tanzania kutangazika kimataifa na kuongezeka kwa makampuni yatakayojihusisha na sekta ya Sanaa

“Mfumo wa digitali una mazuri mengi lakini kubwa ni kuongezeka ushindani na ubora katika kutengeneza maudhui yenye ubora na pia ongezeko la masafa katika televisheni ambayo yatahitaji maudhui (vipindi) ya kutosha” Aliongeza Chacha.
Hata hivyo, aliitaja changamoto ya uharamia kwenye sekta ya Sanaa ambapo aliwashaiuri wasanii kuamka na kujiunga na Chama cha hakimiliki (Cosota) ili kuhakikisha kazi zao zinalindwa kisheria.

Wadau wengi waliochangia mjadala huo walionekana kuwa na wasiwasi na mfumo wa digitali lakini wakaomba elimu ya kutosha itolewe ili wananchi wengi zaidi waelewe nini maana ya kutoka mfumo wa analogia kwenga ule wa digitali.